Kuwahi au kuchelewa kuoa
Sura ya Tatu
- Kuwahi au kuchelewa kuoa
- Wapo watu waliochelewa kuoa ama kuolewa kwa sababu mbalimbali, lakini ni jambo la muhimu sana kufahamu muda mzuri wa kuoa ama kuolewa. Ni watu wachache sana huchelewa kufunga ndoa kwa sababu za msingi. Wengi sababu zao hutokana na uzembe wa kutoipa ndoa umuhimu unaostahili; na hujikuta katika maumivu makali pale wanapoanza kukutana na changamoto za kuchelewa.
- Kadri dunia inavyoendelea kuwepo ndivyo na umri wa kuishi unavyopungua. Wazee wa zamani walifikisha miaka mia tatu hadi mia tisa , uovu ulipoongezeka miaka ikapunguka hadi mia ishirini na baadaye sabini au themanini. Kipindi chetu hiki mtu wa miaka hamsini au sitini sasa ndiye anayeitwa mzee na kama anafanya kazi atastaafu. Mwanzo 5:1-32; Zaburi 90:10. Kipindi watu wanaobahatika kuzidisha miaka hadi tisini na kuendelea maisha yao yanakuwa ya maumivu makali na usumbufu mkubwa kwao na kwa watoto wao; kwa sababu hawezi kujihudumia yeye mwenyewe, huduma zote anategemea zitoke kwa watoto.
- Zipo faida za kuwahi kuoa na hasara za kuchelewa. Kwa kuwa miaka yetu ya kuishi siyo mingi, tunatakiwa tuoe ama tuolewa mapema badala ya kuchelewa; miaka Ishirini na moja hadi Ishirini na sita kwa msichana na ishirini na saba hadi thelathini kwa mvulana. Wanaooana katika miaka hiyo wanapata nafasi ya miaka ishirini na tano ya kuzaa na kumaliza kusomesha watoto wao bado wakiwa na nguvu za kujitegemea. Miaka ishirini na tano inayofuata itatumiwa na watoto wao kuoa au kuolewa na kusomesha wajukuu wao.Hivyo wajukuu wataanza kujitegemea wao wakiwa na miaka kati ya sabini na themanini. Miaka ambayo watakuwa wanahitaji msaada kutoka kwa watoto wao ( kama bado watakuwa hai ); ambao wataupata kwa sababu tayari wajukuu wao hawahitaji msaada wa wazazi wao. Hiyo ni moja wapo ya faida na zipo nyingi, siyo si rahisi kuzisema zote .
- Anayeoa au kuolewa akiwa na miaka thelathini na zaidi kwa msichana au arobaini na zaidi kwa mvulana; ipo hatari ya kukosa kupata watoto kwa sababu umri mzuri wa msichana kuzaa pasipo usumbufu ni kati ya miaka ishirini hadi thelathini na tano. Kama watabahatika kupata watoto, miaka ishirini na tano ya kuzaa na kuwasomesha itakwisha huku wakiwa wameanza kuishiwa na nguvu. Wataanza kutaka msaada wa watoto katika kipindi ambacho bado wanalo jukumu la kuzaa na kuwasomesha wajukuu wao. Hali hiyo itadhoofisha pande zote , sababu wazazi hawatapata msaada wa kutosha na watoto hawatatimiza malengo na mahitaji yao kwa wakati. Hapo ndipo migogoro ya uzeeni iliyosababishwa na wazazi kwa kutokuoa au kuolewa mapema inapoanzia. Katika hali kama hiyo, mzazi anaweza kufariki pasipo hata kumwachia mtoto Baraka.
- Lakini pia lipo tatizo la kuoana huku mna tofauti kubwa ya miaka; mmoja ana miaka arobaini au zaidi na mwingine ana miaka ishirini au zaidi kidogo. Wawili hawa wanatofautiana katika vipaumbele, mitizamo na maono. Wakati mwanamke kama yeye ndiye mdogo atataka watembee maeneo ya muhimu ili awaoneshe wenzake kwamba ameolewa, huku mwanamume anataka akae nyumbani ajisomee vitabu ! Wakati fikira za mwanamke zimejaa mapenzi na mahaba kwa mumewe , yeye anafikiria jinsi ya kutafuta pesa atimize malengo yake ! Mama anataka abadilishe nguo kila wakati, baba anavaa nguo moja kwa siku mbili!
Yamenukuliwa kutoka kitabu; Misingi Inayodumisha Ndoa na Joel M. E.M Chamba uk. 20 - 21
Comments
Post a Comment